Michuano ya ngazi ya vilabu ukanda wa kusini mwa Amerika (Copa Libertadores na Copa Sudamericana), imesimamishwa kwa muda, na huenda ikaendelea tena Mei 05 mwaka huu.
Shirikisho la soka Amerika kusini (CONMEBOL) limethibitisha kusitishwa kwa michuano hiyo, kufutia janga la virusi vya Corona linaloendelea kusambaa kwenye nchi mbalimbali duniani.
Juma lililopita CONMEBOL waliatarajiwa kutoa tamko la kusimamisha michuano hiyo, lakini walikua kimya, kwa kusudio la kuzitaka nchi wanachama kusimamisha ligi zao kwanza.
Mataifa 10 ya ukanda wa kusini mwa Amerika, yamesimamisha ligi zote na huenda zikaendelea tena kati ya Machi 15-21.
Michuano ya Copa Libertadores hushirikisha klabu bingwa katika nchi wanachama za ukanda huo, huku michuano ya Copa Sudamericana ikitambuliwa kama kombe la shirikisho la ukanda wa kusini mwa Amerika.
Kushoto ni taji la Copa Libertadores na kulia ni taji la Copa Sudamericana
Michuano ya Copa Libertadores na Copa Sudamericana inasimama ikiwa imefikia hatua ya makundi na kila timu shiriki imeshacheza michezo miwili.
Michezo ya mwisho ya michuano ya (Copa Libertadores na Copa Sudamericana) ilichezwa Machi 11.
Bingwa mtetezi wa michuano ya Copa Libertadores ni klabu ya Flamengo ya Brazil, na klabu ya Independiente del Valle ya Colombia ndio bingwa mtetezi wa Copa Sudamericana.