Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa ameagiza  Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA),  na Baraza la Sanaa Tanzania  (BASATA), kuandaa mfumo wa kuuza kazi za Wachoraji na Wachongaji kwa njia ya mtandao.

Bashungwa ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam katika kikao chake na Wasanii wa Sanaa ya Uchoraji na uchongaji nchini kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili katika uendeshaji wa kazi zao ikiwemo suala la masoko.

“Katika karne hii ya 21 suala la Masoko linafanyika kwa njia ya mtandao na njia hii ni rahisi na inatangaza biashara kwa haraka zaidi na katika hili COSOTA mtatakiwa kuhakikisha mnalinda Hakimiliki za kazi hizo,” amesema Bashungwa.

Waziri Bashungwa amewasihi Wachoraji na Wachongaji kusajili kazi zao COSOTA ili ziweze kulindwa, huku akitoa msisitizo kwa wadau hao kuhakikisha wanawasiliana  na BASATA pamoja na COSOTA pale wanapokuwa na mikataba yao kibiashara kwa lengo la kupata ushauri wa kisheria ili kuweza kulinda kazi hiyo pamoja na maslahi yake.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi COSOTA, Doreen Sinare ameeleza kuwa taasisi hiyo imetengeneza kanuni mpya ambazo zitawasaidia Wachoraji na Wachongaji kunufaika na kazi zao baada ya kuuza kazi zao na kazi hizo kwenda kuuzwa tena nje ya nchi kupitia minada na njia nyingine kama hizo, ambapo kazi huuzwa kwa bei za juu.

“Napenda kuwasisitiza kuhusu suala la kusajili kazi zenu kuna wakati nilitembelea ofisi za Tingatinga na nikawashauri kuhusu suala la kusajili kazi zenu COSOTA lakini baadhi yenu walikuja ila wengine hawakuja sasa naendelea kuwasisitiza kusajili msisubiri mpaka mnapopata changamoto ndiyo mnaanza kuhangaika,” amesema Doreen.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Adrian Nyamangale ameiomba Serikali kuwa katika zawadi zile za vinyago au picha za kuchorwa zinazotolewa kwa wageni Ikulu basi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataje jina la aliyefanya kazi hiyo pale anapokabidhi, ombi ambalo Waziri Bashungwa amelipokea na kuahidi kulifanyia.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 16, 2021
Azam FC kutumia udhaifu wa Young Africans