Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU) na taasisi ya Ruge Mutahaba Foundation kufanya Kampeni ya kutoa Elimu ya Hakimiliki, inayolenga kutoa elimu kwa wabunifu hasa vijana wanaofanya kazi za Sanaa, Uandishi na Ubunifu.
Akizungumza kuhusu Kampeni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa COSOTA, Doreen Sinare amesema itatambulika kama “HAKIMILIKI YAKO HAILIKI, KAMATA FURSA TWENZETU” kampeni ambayo imezinduliwa hii leo Mei 9, 2024 Jijini Dar es Salaam katika siku ya Maadhimisho ya Miliki Ubunifu Duniani.
Ubunifu huo wa kazi za Sanaa ya Uandishi na Ubunifu unaohusiana na hakimiliki unalindwa na Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 1999, pamoja na marekebisho yake kama ubunifu wa mifumo, Muziki, Filamu, Sanaa za maonesho, Uandishi, Matangazo, Picha na Michoro.
Hata hivyo, makubaliano ya pande hizo mbili yatadumu kwa kipindi cha miaka mitatu na yamelenga kufikia Vijana 1,000,000 na kuongeza usajili wa kazi zinazolindwa na hakimiliki.
COSOTA pia imesema itaendelea kutoa elimu ya hakimiliki, kupitia mkakati wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara (MKUMBI) unaosimamiwa na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwezeshaji chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (European EU).