Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amewataka vijana wabunifu waliokuwa kwenye kampuni changa kutoridhika na kile walichonacho badala yake, waendelee kujifunza kwa kukuza ubunifu walionao.
Dkt. Nungu ameyasema hayo wakati akizungumza na vijana kutoka katika kampuni changa 10 kati ya kampuni 79 zilizotuma maombi ya ushiriki, kwenye mradi wa Kukuza Ubunifu Kusini mwana Afrika (Southern African Innovation Support Program -SAIS, ambapo kwa Tanzania COSTECH ndiyo msimamizi.
Aidha Dkt. Nungu ameelezea lengo la mashindano hayo ni kupata washindi wawili kwenda Nchini Finland kushiriki kwenye mashindano ya Kimataifa ya kutoa mawazo yao kuona kama yanaweza kufadhiliwa na kupata mafunzo zaidi.
Amesema, vijana wengi waliokuwa katika kampuni hizo wanakuwa na mawazo ya kuchangia kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini ndiyo maana tume inawakusanya kwa pamoja ili kuendeleza mawazo yao
“Tulifanikiwa kupata makampuni zaidi ya 10 ambayo yaliweza kushindana na kushinda kwa kupata ufadhili kwa kushirikiana na wenzao katika hilo tunajivunia kampuni ya Arusha na Filter ambao wao walipata ufadhili wa kupeleka teknolojia yao nchini Zambia, kupitia mradi huu wa SAIS,”
Kwa upande wake, muanzilishi na Mwanasayansi wa bahayu kutoka kampuni inayojihusisha na shughuli za uchakataji taka za plastiki kwenda kwenye vifaa vya ujenzi (Arena Recycling Industry,)Hallas David amesema mafunzo ya mradi huo yanayotolewa na Costech yamewawezesha kuweza kufika mbele kwa kuboresha zaidi bunifu zao ili baadae zije kusaidia katika ukuaji wa teknolojia na uchumi nchini.
“Tunafurahi kuona Serikali na SAIS ikiwasaidia vijana wenye mawazo na wabunifu ambao wanatatua changamoto zilizopo ndani ya mazingira yetu na jamii ili kuweza kujiinua kiuchumi na kulipatia Taifa uchumi endelevu,” Amesema David.
Dkt. Nungu amesema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Finland umeanza, 2017 na unawawakilishi kutoka Tanzania, Botswana, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia pamoja na SADC , lengo ni kujenga mifumo ya ubunifu ndani ya nchi zilizokuwepo katika mradi huo na pia kujenga ushirikiano katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.