Jamii nchini, imeaswa kuwekeza katika ubunifu pamoja na kuwasaidia wabunifu watanzania kwa kununua bidhaa zao na kuwapa mrejesho wa ubora wa bidhaa zao, ili kuwatia moyo kama moja ya sehemu ya kuthamini jitihada zao.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia – COSTECH, Dkt. Amosi Nungu wakati akizungumza na waandishi wa Habari kwenye wiki ya Ubunifu kitaifa inayofanyika Viwanja vya Jamhuri, jijini Dodoma.
Amesema, “COSTECH tumewasidia wabunifu wa nyuma kuingia sokoni kunufaika na bunifu mfano mzuri kijana mbunifu wa mita ya maji sasa hivi amepewa tenda na RUWASA kufunga mita nchi nzima kwa hivyo niwaambie tu vijana wanaweza kupata ajira kupitia bunifu zao.”
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inajukumu la kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu lakini maonesho hayo yanaangali zaidi ubunifu kwa upana wake na ndio maana wanawasihi wananchi, taasisi mbalimbali, wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo kwenda kujifunza uwekezaji katika ubunifu.
Dkt. Nungu ameongeza kuwa, “Wananchi wengi wanadhani kwamba bunifu za Tanzania hazidumu yaani tunazionea haya kuzitumia lakini kuona ndo kuamini mfano bunifu ya gari ya kutumia umeme sisi kama taasisi ni kutoa ushauri na maelekezo ili kuweza kuboresha zaidi na kuaminiwa na wananchi.”
“Tumeona bunifu nyingi tu hapa zinazofanywa na vijana zikiwa na utofauti mkubwa sana na bunifu zingine hii ni kuonyesha ni kwa kiasi gani kama nchi tunakuwa katika sekta hii haswa ukizingatia namna ambavyo vijana wanaweza kujiajiri lakini kutoa elimu kisasa na kwenda na wakati haswa kwa wanafunzi mashuleni.” amesema.
Hata hivyo, amewataka Vijana hao kuacha kunakili bunifu za wengine na kubuni vitu vya utofauti, ili waweze kuweka rekodi ya kipekee na kuwa wa kwanza kwenye kuleta tija na ushawishi kwenye jamii.