Timu ya taifa ya Ubelgiji huenda ikakosa huduma ya Mlinda Lango Thibaut Courtois kwenye Fainali za Mataifa ya Ulaya ‘Euro 2024’ kwani ameamua atabaki Madrid aendelee kujiweka fiti baada ya kuumia.
Kwa mujibu wa Radio Marca, Mlinda Lango huyo ameripotiwa kuwafahamisha Madrid kwamba hatasafiri Ujerumani kuiwakilisha Ubelgiji kwa ajili ya michuano Euro 2024, itakayoanza Julai mwakani.
Kipa huyo tegemeo wa Madrid na timu ya taifa, aliumia kabla ya msimu mpya kuanza Agosti, na alifanyiwa upasuaji.
Madrid ililazimika kumsajili kwa mkopo Kepa Arrizabalaga kama mbadala akitokea Chelsea wakati wa usajili uliopita.
Hata hivyo, taarifa hiyo inepingwa vikali ikidaiwa kwamba Courtois atashiriki Euro 2024, endapo atapona haraka jeraha lake.
Wakati huo huo, nahodha huyo wa Madrid ana uhusiano mbaya na kocha wa Ubelgiji, Domenico Tedesco, kwani aligoma kujumuishwa katika kikosi cha Ubelgiji Juni mwaka huu.
Imeelezwa Mlinda Lango huyo mwenye umri wa miaka 31, alitofautiana kauli hadharani na kocha wa Ubelgiji baada ya Romelu Lukaku kuvuliwa unahodha kabla ya mechi ya kufuzu Euro 2024 dhidi ya Austria.
Kwa mujibu wa meneja huyo, Courtois alichukizwa baada ya Lukaku kuvuliwa unahodha ndo maana ameamua kujiondoa kikosini.
Tangu Courtois alipoumia Koen Casteels amechukua nafasi yake katika kikosi cha Ubelgiji, na huenda akawa chaguo namba moja.
Katika hatua nyingine Courtois anaaamini atarejea dimbani kwa ajili ya msimu wa 2024-25.