Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imepokea ndege ya kwanza itakayotua na skana za EDE zenye uwezo wa kutambua uwezekano wa maambukizi ya Uviko-19 kupitia Skamu ya Umeme kwa kutumia simu ya mkononi.
Mapokezi ya skana hizo za kipekee barani Afrika, yanaiweka Tanzania kama nchi ya kwanza kihistoria kutumia Teknolojia hii, katika mapambano dhidi ya Janga la COVID-19.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya mapokezi ya Skana hizo, zinazoingizwa nchi kupitia shirika la Sanimed International kwa kushirikiana n Alfa Care, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema teknolojia hiyo itawapa afueni maelfu ya watalii ambao watapata urahisi kuendelea kuingia visiwani humo kwa njia iliyo salama.
Amesema licha ya kuwa Zanzibar ni salama na kuanzia mwezi Januari hadi Februari 2022 Zanzibar haijaripoti kisa kipya cha Uviko-19, hawapaswi kubweteka dhidi ya kupambana na kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo hatari duniani.
Kwa upande wake, Meneja Mradi kutoka Sanimed, Dk. Mohammad Gulrez amesema teknolojia hiyo ni salama kwa afya ya binadamu, na kwamba inaokoa muda wa kusubiri majibu ya vipimo.