Imefahamika kuwa Klabu ya CR Belouizdad ya Algeria, imemtengea Simon Msuva ofa ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.5 kuinasa saini ya nyota huyo aliye huru kwa sasa.
Msuva ambayė mkataba wake wa kuitumikia Al-Qadsiah FC ya nchini Saudi Arabia ulimalizika Julai 1, 2023, kwa sasa hana timu, huku akiwa amefanikiwa kuzitumikia klabu kadhaa za Ukanda wa Afrika Kaskazini ikiwemo Difaa El Jadida na Wydad Cassablanca.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, tayari Msuva ameondoka nchini na kuelekea Algeria kwa ajili ya kujiunga na CR Belouizdad kwa dau hilo la zaidi ya shilingi bilioni l.5.
“Sasa naweza kukuambia rasmi kuwa, Msuva amepiga chini ofa za Simba SC na Young Africans, baada ya kupata dili kubwa nchini Algeria, ambapo awali Young Africans walimpatia ofa ya Shilingi Milioni 350 na mshahara wa Shilingi Milioni 20 kila mwezi.
“Simba SC wao wakampatia ofa ya Shilingi Milioni 400 na Mshahara wa Shilingi Milioni 25 kila mwezi, ambapo aliwaambia wasubirie atawajibu jambo ambalo limekwama baada ya CR Belouizdad kuingilia dili hilo na kumuhakikishia mshahara wa zaidi ya Shilingi Milioni 50 kila mwezi, huku wakiweka mezani ofa ya zaidi ya Shilingi Bilioni Moja.
“Tayari Msuva amekwea ndege usiku wa kuamkia leo (jana Jumatano) Agosti 23 tayari kwa ajili ya kwenda kukamilisha dili hilo akiwa sambamba na uongozi unaomsimamia, ” kimesema chanzo hicho.