Benki ya CRDB imefanya marekebisho makubwa kwenye suala zima la mikopo inayotolewa na benki hiyo ambapo wameamua kushusha kiwango cha riba kwa wateja wote toka asilimia 22 hadi asilimia 16 na mkopo kuweza kutolewa ndani ya masaa 24 mara baada ya mteja kukidhi vigezo vyao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Benki hiyo, Charles Kimei ambae ametaja lengo kubwa la kufanya marekebisho hayo ni kwawezesha watanzania kufanya chochote ili kuongeza kipato chao na kuboresha maisha yao.
Mbali na hilo Kimei ameongezea kuwa CRDB imeboresha viwango vya mkopo kutoka Milioni 50 hadi Milioni 100 lengo likiwa kuwawezesha wateja wao kupata mkopo mkubwa wa kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo.
Aidha kubwa kuliko yote Kimeo amesema kuwa boresho lingine lililofanyika ni kuongeza muda wa kurejesha fedha hizo ambapo hapo awali fedha zilikuwa zikirejeshwa ndani ya miaka mitano lakini kwa sasa wameongeza mpaka miaka saba.
Ambapo kwa kufanya hivyo inamuwezesha mkopaji kukatwa kiwango kidogo cha fedha tofauti na awali ambapo wateja walikuwa wakikatwa kiwango cha juu kidogo cha fedha ili kukidhi muda maalumu ulioweka wa kufanya marejesho ya fedha hizo.
Aidha amewataka wateja wao kutumia fursa hiyo ili waweze kukopa na kufaidi maboresho yalifanywa na CRDB na kufurahia mikopo yao na kuilipa bila wasiwasi, pia amewataka wateja wa benki nyingine kuhamia CRDB kwani kwa sasa wanauwezo wa kununua mikopo kutoka benki nyingine.