Hatimae uongozi wa klabu ya AC Milan, umemfungashia virago Sinisa Mihajlovic, baada ya kuchoshwa na huduma yake ya ukufunzi tangu alipokabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi cha The Rossoneri mwanzoni mwa msimu huu.

Maamuzi hayo ya AC Milan yamekuja ikiwa ni baada ya mwezi mmoja kupita ambapo baadhi ya vyombo vya habarti nchini Italia, viliibua tetesi za kufukuzwa kazi kwa Mihajlovic, lakini haikua hivyo.

Matokeo ya kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi ya nchini Italia, Juventus mwishoni mwa juma lililopita, yamechangia kwa kiasi kikubwa kufukuzwa kwa meneja huyo kutoka nchini Montenegro.

Tayari viongozi wa AC Milan wameshamtaja Cristian Brocchi kuwa mbadala wa Mihajlovic, baada ya kumfanyiwa tathmini na kuonekana anaweza kufikia lengo lililowekwa hadi mwishoni mwa msimu huu.

Brocchi ametajwa kushika wadhifa huo, akitokea kwenye kikosi cha vijana cha AC Milan kama kocha na falsafa ya klabu hiyo inaaminika itamuongoza katika shughuli zake hadi mwishoni mwa msimu huu.

   Meneja aliyefutwa kazi Sinisa Mihajlovic

Kwa sasa AC Milan wapo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ya Sirie A, kwa kufikisha point 49 ikiwa ni tofauti ya point 30 dhidi ya vinara Juventus wenye point 79 huku michezo sita ikisalia kabla ya msimu wa 2015-16 haujafikia kikomo.

Endapo Brocchi atafanya kazi yake ipasavyo na kufanikisha azma ya kushinda michezo yote sita iliyosalia, AC Milan itafikisha point 67 ambazo huenda zikawapeleka kwenye michuano ya kimataifa msimu wa 2016-17.

Mchezo wa kwanza kwa Brocchi utachezwa mwishoni mwa juma hili kwa kushuhudia kikosi cha AC Milan kikipambana na Sampdoria huko mjini Genoa, katika uwanja wa Luigi Ferraris.

Michezo mingine itakayofuatia baada ya huo wa mwishoni mwa juma hili, AC Milan watapambana na Carpi, Hellas Verona, Frosinone, Bologna na kisha kufunga msimu dhidi ya AS Roma.

Cristian Brocchi, aliwahi kuitumikia klabu ya AC Milan kuanzia mwaka 2001–2008, baada ya kusajiliwa kutoka Inter Milan na kufanikiwa kutwaa mataji ya nchini Italia pamoja na barani Ulaya.

Ifuatayo ni orodha ya mataji aliyotwaa Brocchi akiwa na AC Milan

  • Serie A: 2003–04
  • Coppa Italia: 2002–03
  • UEFA Champions League: 2002–03, 2006–07
  • FIFA Club World Cup: 2007
  • UEFA Supercup: 2003, 2007

TFF Yawashukuru Wadau, Viongozi, Wachezaji Na Mashabiki
Mayweather apinga ushindi wa Pacquiao kwa Brandley, amtaka Brandley afanye hili