Mshambuliaji Chipukizi, Cristiano Jr (mtoto wa Cristiano Ronaldo) amerejea katika shule ya vipaji ya Real Madrid kutoka Manchester United ikiwa ni miaka minne tangu aondoke klabuni pamoja na baba yake.
Cristiano Jr ametimkia Real Madrid siku chache baada ya babake kuonekana kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Real Madrid wakati akiendelea kutafuta klabu mpya.
Akiwa na umri wa miaka 12 tu Cristiano Jr amekuwa akichezea kikosi cha Manchester United U-14 akifunga magoli 58, Assists 18 katika mechi 23.
Hata hivyo haijathibitishwa kama ataendelea kuwa sambamba na Baba yake Mzazi, ambaye anatajwa kuwa mbioni kutimkia Saudi Arabia, kufuatia kuhusishwa na Klabu ya Al Nassr.
Uongozi wa Manchester United na Ronaldo walikubali kuvunja Mkataba siku chache baada ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar, kufuatia kauli tata zilizotolewa na Mshambuliaji katika moja ya Chombo cha Habari Barani Ulaya akiishutumu Klabu hiyo.
Maamuzi ya kuvunjwa kwa Mkataba wa pande hizo mbili yalimuathiri hadi Cristiano Jr, ambaye alilazimika kuondoka kwenye kikosi cha vijana na Manchester United.