Mtoto wa nyota wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, ‘Cristiano Jr amejiunga na timu ya vijana ya klabu hiyo chini ya umri wa miaka 15.
Hiyo ni hatua nyingine ya kisoka katika maisha ya mtoto huyo wa Ronaldo ambaye amekuwa akihamia kila timu baba yake anakokwenda na anatamani siku moja acheze sambamba na baba yake.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usajili Fabrizio Romano, alisema Cristiano Jr mwenye umri wa miaka 13, atafuata nyayo za baba yake na atavaa jezi yenye namba saba kama baba yake.
Baba yake alisaini katika kikosi cha wakubwa Januari na amekuwa hatari tangu alipotua kwenye klabu hiyo.
Sasa Christiano Jr ana matumaini ya siku moja atacheza na baba yake katika ngazi ya kimataifa na klabu kwa jumla atakapofikisha umri wa miaka l6.
Mtoto wa mshindi huyo mara tano wa Ballon dO’r alifichua matarajio ya tangu mwaka jana 2022 alisema: “Baba vumilia miaka michache ijayo nitacheza pamoja na wewe.”
Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid ana umri wa miaka 38 na anapambana kuwa fiti ili kutimiza ndoto za mtoto wake ambaye wamefanana kila kitu.
Ripoti zimedokeza Ronaldo anatamani kucheza Kombe la Dunia mwaka 2026 na ataendelea kukipiga Al-Nassr hadi michuano itakapofika.
Mtoto wa Ronaldo amepita katika timu za vijana za klabu kama Manchester United, Madrid, Juventus na sasa Al-Nass.