Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu suala la kuihama klabu ya Real Madrid na kujiunga na mabingwa wa soka nchini Italia – Juventus.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 amefunguka suala hilo alipohojiwa na mwandishi wa habari wa DAZN, ambapo alisema ilikuwa ni rahisi kufanya maamuzi ya kuondoka mjini Madrid na kutua mjini Turin yalipo makao makuu ya klabu ya Juventus.
Hata hivyo, Ronaldo alisema hakuwa amepanga kucheza soka katika klabu ya Juventius katika maisha yake, lakini hali hiyo ilitokea kutokana na hitaji lake la kutaka kubadili mazingira, hasa baada ya kukaa na Real Madrid kwa kipindi kirefu.
Alisema anaamini ulikua muda sahihi wa kuondoka Real Madrid baada ya kuona hana suala jipya la kufanya ndani ya klabu hiyo, kutokana na kutoa mchango mkubwa ambao ulipelekea kupatikana kwa mafanikio ya kutwaa mataji ya barani Ulaya na duniani kwa ujumla.
“Ninaamini baadhi ya mashabiki wanajua huenda hatua ya kuhama ilinipa wakati mgumu kufanya maamuzi ya kuondoka Real Madrid, lakini haikua hivyo. Ilikua ni maamuzi rahisi mno, nilitambua muda niliokaa Stantiago Bernabeu ulikua umekwisha,” alisema.
“Sikuwa na matarajio ya kuitumikia Juventus katika maisha yangu, japo nilipanga kuondoka Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita, suala la kuja hapa limetokana na mazingira ya kimaisha,” aliongeza.
“Ilinishangaza hata mimi kuona nimetua Juventus, kutokana na mambo ya uhamisho wangu yalipokua katika hatua za awali kabisa, wakala wangu alishughulikia jambo hili hadi lilipokamilika na kutangazwa katika vyombo vya habari, lakini sikuwa nafahamu kama ingetokea mimi kuja hapa,” anakaririwa zaidi.
Hata hivyo Ronaldo alisema amejiwekea dhamira kubwa ya kuendelea kutwaa mataji akiwa na klabu ya Juventus, huku akisisitiza kuhitaji taji la ligi ya mabingwa barani Ulaya, ambalo kwa mara ya mwisho alilipigania akiwa Real Madrid na kufanikiwa.
“Ninategemea kuandika historia mpya nikiwa na Juventus, ninataka kutwaa mataji zaidi nikiwa hapa. Ninatamani kutwaa tena taji la ligi ya mabingwa barani Ulaya nikiwa na Juventus, ninaamini suala hilo linawezekana kutokana na timu hii kuwa na kikosi imara.”
Kwa mara ya mwisho Juventus kutwaa ubingwa wa Ulaya ilikua mwaka 1996, na baada ya hapo wamewahi kuwa washindi wa pili mara tano.
Ronaldo alijiunga na mabingwa hao wa Italia kwa ada ya Pauni milioni 105 mwazoni mwa mwezi Julai, baada ya kuitumikia Real Madrid kwa miaka tisa mfululizo.