Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo, ameonekana akifanya mazoezi binafsi katika Uwanja wa Klabu yake ya zamani Real Madrid, ili kujiweka Fit, baada ya kurejea kutoka nchini QATAR.
Roaldo alishindwa kuisaidia Ureno kufanya vizuri katika Fainali za Kombe la Dunia 2022, na kujikuta ikiondolewa kwenye hatua ya Robo Fainali kwa kufungwa na Morocco 1-0.
Ronaldo alionekana akifanya maozezi binafsi katika kambi ya Real Madrid ya Valdebebas, lakini hali hiyo haimaanishi kama ana nafasi ya kurejea tena klabuni hapo.
Kufuatia mkataba wake na Klabu ya Manchester United kusitishwa mapema mwezi uliopita, Mshambuliaji huyo anatarajia kuanza maisha mapya akiwa na klabu nyingine mapema mwezi Januari 2023.
Klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia imekua ya kwanza kuonesha nia ya kumsajili Ronaldo mwenye umri wa miaka 37, ingawa inafahamika kuwa bado ana ana uwezo wa kufanya maamuzi mengine tofauti.
Klabu ya Manchester United ililazimika kusitisha mkataba wa Ronaldo, baada ya mahojiano yenye utata ambapo mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or aliikosoa klabu hiyo na kusema meneja Erik ten Hag hajawahi kumpa heshima yake.
Mahojiano hayo yalifanyika siku mbili kabla ya Ureno kuanza kampeni ya Kombe la Dunia na Ronaldo kuanza michezo yao mitatu ya kwanza, akijibu kwa hasira alipotolewa katika mchezo wa mwisho wa Hatua ya Makundi dhidi ya Korea Kusini.
Shirikisho la Soka la nchini Ureno lilikanusha kuwa Ronaldo alitishia kuondoka kwenye kikosi hicho baada ya kuambiwa hataanza mchezo wa Hatua ya 16 bora dhidi ya Uswizi, na badala yake Goncalo Ramos alifunga Hat-Trick katika ushindi wa mabao 6-1.