Ndoto za mshambuliaji kutoka nchini Ureno, Luís Carlos Almeida da Cunha (Luis Nani) za kucheza soka nchini England kwa mara ya pili zimeota mbawa baada ya uongozi wa klabu ya Valencia kufanikisha mpango wa kumsajili akitokea Uturuki alipokua akiitumikia Fenerbahce.

Valencia wamethibitisha na kumtambulisha Nani mbele ya waandishi wa habari kufuatia taratibu zote za uhamisho wake zilizogharimu kiasi cha Pauni milioni 7.2 kukamilishwa rasmi.

Mshabiki zaidi ya 10,000 nao walishiriki katika utambulisho huo ambao baadae ulihamia katika uwanja wa Mestalla.

Mshambuliaji huyo ambaye bado anatembea kifua mbele kutokana na kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya kilichotwaa ubingwa wa barani Ulaya (Euro 2016) mwishoni mwa juma lililopita, amesema amefurahishwa na uhamisho huo na anaamini utamfungulia ukurasa mpya wa upinzani katika soka lake.

Hata hivyo Nani amepasua ukweli wa kilichomvutia na kuamua kujiunga na Valencia kwa kumtaja mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

Amesema wakati wakiwa katika fainali za mataifa ya barani Ulaya (Euro 2016), mshambuliaji huyo na nahodha wa Ureno alitumia muda mwingi kumshawishi kwa kumuelezea mazingira ya soka la nchini Hispania, na hatimae alivutiwa na kufikia maamuzi ya kujiunga na klabu hiyo ambayo kwa mara ya mwisho ilitwaa ubingwa wa La Liga msimu wa 2013-14.

Klabu ya Everton iliwahi kuhusishwa na mpango wa kutaka kumsajili Luis Nani, siku chache baada ya uongozi wa The Toffees kusaini mkataba na meneja kutoka nchini Uholanzi Ronald Koeman.

Nani aliwahi kuitumikia klabu ya Man Utd ya nchini England kuanzia mwaka 2007–2015, lakini msimu wa 2014715 alipelekwa kwa mkopo Sporting Lisbon ya Ureno kabla ya kuuzwa moja kwa moja kwenye klabu ya Fenerbahce ya nchini Uturuki.

Video: Matokea Kidato cha Sita 2016 Yatangazwa
Mikoa 5 Kupatiwa Huduma za Afya Bure na Madaktari Bigwa Kutoka China