Mshambuliaji zamani wa FC Barcelona na Timu ya Taifa ya Brazil, Rivaldo Vitor Borba Ferreira, amemtaka Cristiano Ronaldo kurejea Real Madrid ili kumalizia soka lake kwa heshima.
Rivaldo amedai kuwa Cristiano Ronaldo huenda alidanganywa na dili lake la Al-Nassr ya Saudi Arabia ambapo alisaini mkataba wa pauni milioni 173 kwa mwaka.
Rivaldo amependekeza kuwa ni wakati wa Ronaldo kurejea Real Madrid kwani alipo sasa siyo sehemu ambayo inaendana na hadhi yake.
“Ronaldo angeweza kudanganywa aliposaini mkataba wake mkubwa na Al-Nassr,” amesema Rivaldo
Ronaldo, 38, alijiunga na timu hiyo ya Saudi Arabia Januari mwaka huu baada ya kandarasi yake na Manchester United kukatishwa kufuatia mahojiano makali yaliyoikosoa klabu hiyo.
Aidha nyota wa Brazil, Rivaldo amependekeza mishahara mikubwa inayotolewa Saudi Arabia inaficha ugumu wa ligi na mtindo wa maisha katika jimbo hilo la Ghuba.
“Ninaelewa kwamba wakati mwingine wachezaji hupumbazwa na mikataba mikubwa wanayosaini Saudi Arabia, lakini maisha huko yanazidi kufungwa na soka si rahisi kama inavyotarajiwa,” amesema.
Kumekuwa na taarifa zinazodai kuwa Madrid wamefanya makubaliano yenye manufaa na Ronaldo ili kurejea klabuni hapo msimu ujao.