Rais wa klabu ya CSKA Moscow Evgeniy Giner amesema mpaka sasa hawajapokea ofa kutoka Chelsea kwa ajili ya kiungo Aleksandr Sergeyevich Golovin, ambaye aling’ara na timu ya taifa ya Urusi wakati wa mshike mshike wa fainali za kombe la dunia zilizofikia tamati mwishoni mwa juma lililopita.
Giner ameweka wazi taarifa hizo, kufuatia vyombo vya habari vya England kuripoti kuwa, klabu ya Chelsea imefanikisha lengo la kukaribia usajili wa Golovin.
Kiongozi huyo amesema wameshtushwa na taarifa hizo, ambazo amedai huenda zilipikwa makusudi, lakini akaendelea kusisitiza mpaka sasa hawajapokea ofa yoyote kutoka kwa The Blues, ambao wapo chini ya meneja mpya kutoka Italia Maurizio Sarri.
Hata hivyo Giner amewataka viongozi wa Chelsea kufuata utaratibu endapo wanahitaji huduma ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
“Tumeshtushwa na taarifa hizi, lakini ukweli ni kwamba hakuna ofa tuliyoipokea kutoka Chelsea, ninawashauri viongozi wao waje tuzungumze ili tuangalie kama tutaweza kufanya biashara ya uhamisho wa mchezaji huyu, ambaye ninatarajia atakua staa siku za karibuni. ”
“Hatuna nia ya kumzua Golovin, tunataka afanikiwe kadri atakavyopata nafasi, lakini yote hayo yatapewa nafasi kama upande unaoonyesha nia ya kumsajili utafuata taratibu za uhamisho,” alisema Giner alipohojiwa na tovuti ya Sport24.
“Tukipokea ofa, tutawajulisha na tutatoa taarifa za kila hatua tutakayokua tunaipiga katika mazungumzo na upande utakaokua tayari kumsajili Golovin.
Mbali na klabu ya Chelsea kuonyesha nia ya kumsajili Golovin, klabu nyingine zinazotajwa kuwa kwenye mkakati huo ni Arsenal, AS Monaco na Juventus.
Golovin alifanikiwa kucheza michezo mitano katika fainali za kombe la dunia akiwa na timu ya taifa ya Urusi, na alifunga moja ya mabao yaliyoipa ushindi timu hiyo katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Saudi Arabia, waliokubali mabao matano kwa sifuri.