Miguel Diaz-Canel ameapishwa rasmi kuwa rais mpya wa Cuba akichukua nafasi ya Raul Castro ambaye alishika madaraka hayo mwaka 2006 kutoka kwa kaka yake na mwanamapinduzi wa taifa hilo, Fidel Castro.
Hii ni mara ya kwanza kwa familia ya Castro kutohusika na nafasi hiyo ya juu zaidi nchini humo tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Fidel mwaka 1959.
Diaz-Canel ambaye alikuwa makamu wa rais wa taifa hilo kwa miaka mitano, alikuwa mmoja kati ya watu wa karibu zaidi ya familia ya mwanamapinduzi Fidel Castro, hususan Raul.
Mwanasiasa huyo ameshika nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa na bunge mwezi Machi mwaka huu kwa kura 605 ambazo ni karibu idadi ya kura zote zilizopigwa. Alitangazwa kuwa mshindi kwa asilimia 99.8.
Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza, Diaz-Canel amesema kuwa atahakikisha anadumisha mapinduzi ya nchi hiyo na sera zake ili kuweka historia katika mahala salama.
Kiongozi huyo mpya wa Cuba amesema kuwa Cuba itabaki kuwa kisiwa pekee chenye kufuata mfumo wa kuwa na chama kimoja na kudumisha sera za Kikomunisti.
Ingawa Raul ameachia madaraka, bado anakuwa ndiye kiongozi na mwenye ushawishi zaidi katika chama cha The Communist Party.