Siku moja baada ya Mkutano Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) ulioitishwa jijini Dar e Salaam kumchagua tena Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad umeibuka kuupinga.
Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande amesema kuwa mkutano ule ni batili na kila kilichofanyika ni batili ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho ni batili.
Amesema kuwa Mahakama Kuu ilitoa maamuzi ya kuzuia kufanyika kwa mkutano huo tangu Februari 28, na kwamba kilichofanyika kilikuwa kukaidi amri ya Mahakama.
“Ubatili wa Mkutano ule unatokana na maamuzi ya Mahakama Kuu ambao umetolewa Februari 28 mwaka huu, katika shauri ambalo Nassor Ahmed Mazrui na mwenzake wamelifungua kupinga kufanyika kwa Mkutano Mkuu kwa sababu tetesi za kufanyika mkutano ule zilifanyika tangu mwaka jana,” Maharagande ameiambia Global TV, leo.
Amesema kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu ambao alionesha nakala yake, ulitolewa na Jaji Steven Magoiga kuhusu shauri lililofunguliwa mahakamani Nassor Mazrui na mwenzake.
“Kama mkutano uliofanyika ni haramu kisheria kama nilivyokuonesha nakala ya Mahakama hapa, maamuzi yake hayawezi kuwa halali, lazima nayo ni haramu,” amesema Maharagande.
Maharagambe ameeleza kuwa chama hicho hadi sasa hakina Mwenyekiti na kwamba kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, Mkutano Mkuu wa kufanya uchaguzi huo unapaswa kufanyika Juni mwaka huu na kwamba Baraza Kuu ndilo lililopewa mamlaka ya kuongeza muda usiozidi miezi sita endapo itaona inafaa ili Mwenyekiti achaguliwe.
Jana, Profesa Lipumba ambaye ndiye Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, alichaguliwa kwa kishindo akipata kura 516, sawa na asilimia 88 ya kura zote zilizopigwa.
Profesa Lipumba aliwashukuru wanachama wa chama hicho kwa kuendelea kumuamini na kuahidi kuendelea kukitumikia chama hicho na kuhakikisha msimamo wake wa haki sawa kwa wote unaendelea kutekelezwa kwani unawavutia wananchi wengi.