Chama Cha Wananchi (CUF) kimepanga kutoa majibu ya kina kuhusu uamuzi wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wake.

Akiongea na waandishi wa habari muda mchache baada ya Profesa Lipumba kutangaza uamuzi wake, Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa alithibitisha kupokea barua ya profesa Lipumba kuhusu uamuzi wake na kuongeza kuwa chama hicho kitatoa majibu ya kina Jumapili, Agost 9.

Jussa alieleza kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif ameagiza uongozi wa chama hicho kukutana siku hiyo ili kujadili na kutoa muongozo kufuatia uamuzi wa Profesa Lipumba na namna ya kumchagua mwanachama mwingine kuziba nafasi hiyo ya juu zaidi ya chama hicho.

Ingawa alikiri kuwa kuondoka kwa Profesa Lipumba katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ni pigo kwa chama hicho, Jussa alisisitiza kuwa chama hicho kamwe hakitayumba kwa kuwa kimepitia mengi hadi hapo kilipofika.

“Pamoja na ukweli kwamba kuondoka kwa Profesa Lipumba katika safu ya uongozi utaacha pengo hasa kwa kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, lakini tunawahakikishia wanachama na wapenzi wa Chama cha Wananchi (CUF) na watanzania kwa ujumla kwamba chama hiki hakitayumba,” Jussa alieleza.

Jussa alisisitiza kuwa hakuna ugomvi wowote ndani ya Chama hicho unaoweza kuhusishwa na uamuzi wa Profesa Lipumba.

Akielezea uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema kuwa kutokana na kutofautiana mtazamo na baadhi ya viongozi wa chama hicho, amekuwa akionekana kama kikwazo.

Aliongeza kuwa ingawa alishiriki katika maamuzi yote ya Ukawa kumpata mgombea mmoja wa urais, dhamira yake imekuwa ikimsuta.

“Dhamira na nafsi inanisuta, inakuwaje kiongozi ambaye alipitisha katiba hii [iliyopitishwa na bunge la katiba] awe kiongozi mkuu halafu asimamie katiba hii [Ya Jaji Warioba]. Nimejitahidi sana kuvumilia lakini nafsi inanisuta, nimeshindwa,” alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alisisitiza kuwa atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa Chama Cha Wananchi (CUF) na amepanga kujihusisha na shughuli za kitaaluma na kufanya utafiti kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya taifa.

Ikumbukwe kuwa profesa Lipumba ni mchumi anaeaminika sana duniani na aliwahi kuwa kati ya maprofesa watano waliochaguliwa kuishauri Namibia kuhusu uchumi wao, lakini pia anafundisha vyuo zaidi ya vinne vya kimataifa.

 

Kim Kardashian, Kanye West ‘Waselfika’ Na Hillary Clinton
Spurs Wajitutumua Kwa Charlie Austin