Baadhi ya wabunge wa Chama cha wananchi (CUF), wameonesha nia ya kukubaliana na pendekezo la wazee wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa Maalim Seif anaweza kuhamia chama hicho na kugombea urais wa Zanzibar 2020.

Mbunge wa Malindi kwa tiketi ya CUF, Ali Salehe amesema kuwa hakuna kinachoshindikana na kwamba endapo mgogoro ndani ya chama hicho utaendelea hadi wakati huo, anaweza kuhamia chama chochote cha upinzani.

CUF ni mwanafamilia wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaundwa na vyama vingine vya upinzani vya Chadema, NCCR Mageuzi pamoja na NLD.

Maoni hayo ya Salehe, yametokana na gumzo lililoibuka kufuatia kauli ya Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema, Hashim Juma na tamko la Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Vicent Mashinji aliyesema watajadili kuhusu maoni hayo muda ukifika.

“Ukishauriwa na wazee ni muhimu kukaa na kujadili kwanza huo ushauri wao na hakuna anayeweza kuukataa. Cha muhimu ni kujua malengo yake tu na wala sio vingine,” alisema Dkt. Mashinji.

Hata hivyo, ingawa Maalim Seif ambaye aliingia kwenye mgogoro wa madaraka na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, amewahi kuweka msimamo kuwa hana mpango wa kuihama CUF.

Mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho umesababisha mpasuko mkubwa, na kutengeneza timu mbili, moja inayomuunga mkono Maalim Seif na ile inayomuunga mkono Profesa Lipumba.

Hali imekuwa tofauti zaidi baada ya Julius Mtatiro, aliyekuwa amepewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi akimuunga mkono Maalim Seif kutimkia CCM.

Kubenea awavuruga Chadema
Aliyerudisha Musoma Hotel kwa Serikali apewa kibano kingine