Chama cha Wananchi (CUF) kimetoa majibu kuhusu taarifa zilizoenea kuwa chama hicho kimejitenga na umoja wa vyama vya siasa vinavyounda UKAWA, vilivyo na nia ya kumsimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu.
Taarifa zilizodai kuwa chama hicho kina mpango wa ujiengua na Ukawa zilichochewa zaidi na kutohudhuria kwa chama hicho katika mkutano wa Ukawa na waandishi wa habari uliofanyika jana.

Akiongea na Radio One Stereo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Bi. Magdalena Sakaya alisema kuwa taarifa hizo sio za kweli na kwamba kutohudhuria kwao kwenye kikao hicho kulitokana na kuwepo shughuli muhimu za ndani ya chama hicho zilizoingilia na ratiba ya kikao hicho. Aliongeza kuwa alimtumia taarifa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kumueleza sababu za kutohudhuria kwao.

Bi. Sayaka pia alikanusha taarifa kuwa Ukawa wameshindwa kuelewana kumsimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais.
“Hapana, kwa sababu malengo yetu tangia mwanzo. Unakumbuka umoja wetu ulianzia bungeni kwenye bunge la katiba, lakini tulikuja kukubaliana kuingia umoja kwenye serikali za mtaa na tukasema tunaangalia uwezekano wa kwenda pamoja kwenye uchaguzi mkuu ujao. Kwa hiyo sio kwamba ni kitu ambacho kimeibuka leo. Misuguano sisi na Ukawa hakuna, lakini sisi tunatakiwa kufuata utaratibu wa ndani ya chama,” alisema Bi. Sakaya.

Aliongeza kuwa wanachama wa chama hicho wamekuwa na msukumo wa kuhoji kwa kuwa viongozi wa CUF walikuwa wanakiuka katiba yao ambapo wanachama hao walisikia kwenye vyombo vya habari kuwa Ukawa wameshampata mgombea wa urais kabla chama hicho hajifanya maridhiano na taratibu za ndani.

Katika hatua nyingine, Ukawa wamekanusha taarifa za kufanya vikao vingi na kushindwa kuafikiana kuhusu kumsimamisha mgombea mmoja. Viongozi wa chama hicho wameeleza kuwa wamelazimika kufanya mikutano zaidi hasa baada ya kuongezeka kwa majimbo ya uchaguzi, hivyo wanakubaliana jinsi ya kuwasimamisha wagombea wao.

Awali, ilidaiwa kuwa umoja huo umekuwa ukivutana kuhusu jina la mgombea atakaewawakilisha, huku majina ya Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) na Dr. Wilbrod Slaa (Chadema) yakiwa chanzo cha mtafaruku.

Kingunge: Kamati ya Maadili CCM haina maadili
Maradona Amshauri Messi