Wakati mazungumzo ya kutatua mgogoro uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yakiendelea, vyama vya CUF na CCM vimezua sintofahamu kwa wananchi baada ya kupingana kuhusu taarifa ya kinachoendelea katika mazungumzo hayo.

Siku moja baada ya kamati maalum ya CCM iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Dk. Ali Mohamed Shein kueleza kuridhishwa na hatua za mazungumzo yanayoendelea huku ikiwataka wanachama wake kujiandaa na marudio ya uchaguzi, CUF imetoa taarifa yake kupinga kilichoelezwa huku ikiwasisitiza wafuasi wake kusubiri kutangazwa kwa matokeo halali ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jusa alisema kuwa kauli iliyotolewa na CCM ni ya chama kinachoshindwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano (CUF), Jusa Salim Jusa

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano (CUF), Ismail Jusa

“CUF inawahakikishia wazanzibari kwamba haitateteleka na itasimamia kwa dhati maamuzi hayo waliyoyafanya kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, na italinda chaguo lao la rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani wao,” alisema Jusa.

Jusa aliongeza kuwa mazungumzo yanayoendelea kati ya aliyekuwa mgombea wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na Dk. Ali Mohamed Shein (CCM) wakiongozwa na viongozi wa ngazi za juu wa chama na Serikali yako katika hatua nzuri za mwisho. Aliwataka wazanzibar kusubiri taarifa rasmi ambayo alidai ni tofauti na kinachoelezwa na CCM.

“Tunawaambia wazanzibar wasubiri taarifa rasmi ya matokeo ya mazungumzo yanayowahusisha viongozi wakuu wa kisiasa ambayo yako katika hatua za mwisho kumalizika. Na hili tuseme dhahiri hapa, siku moja kabla ya kikao cha kamati maalum ya CCM kwa upande wa Zanzibar, nafikiri sote tulimshuhudia Dk. Ali Mohamed Shein akiwepo ikulu ya Dar es Salaam.

“Alizungumza na waandishi wa habari. Hakuzungumzia marudio ya uchaguzi, badala yake alisema wananchi wasubiri mazungumzo yamalizike na baada ya hapo taarifa rasmi itatolewa,” Jusa alieleza.

 

Lukuvi aagiza watumishi kufanya kazi hadi Usiku, Abaini Urasimu Mkubwa Wizarani
Wawili Mbaroni Kwa kupanga Shambulizi la Kigaidi Mkesha wa Mwaka Mpya