Msajili wa Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), Dkt. David Mnzava, amemtaka daktari wa kituo cha Afya cha Kerege kilichopo Mkoani Tanga, Jackson Meli aliyefumua nyuzi kwenye jeraha la mgonjwa kutoa maelezo ndani ya siku 14,
MCT imetoa notisi ya uchunguzi wa awali ya kuwasilisha kwa maandishi utetezi wake katika muda wa siku 14 kwa mujibu wa Kanuni ya 7(1) (b) ya kanuni ya uendeshaji wa mashauri ya Udaktari.
”Baada ya kupokea taarifa hii rasmi baraza linaendelea na hatua za kimaadili kuhusu shauri tajwa na hatua kali kwa mujibu wa sheria ya Udaktari, Udaktari wa meno na Afya shirikishi sura Na.152 ya mwaka 2017, zitachukuliwa baada ya mtuhumiwa kukutwa na hatia” amesema Dkt. Mnzava
Dkt. Mnzava amesema shauri tajwa limethibitishwa na mamlaka ya usimamizi wa Mkoa ambayo ni Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kwa barua yenye kumbukumbu namba RM/D.10/24 ya septemba 6, 2021.
Aidha ametoa wito kwa wataalamu na wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya kuwasilisha taarifa za wagonjwa wasio na uwezo wa kuchangia huduma za afya kwa maofisa ustawi wa jamii katika vituo na maeneo husika kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu huduma za msamaha.
Itakumbukwa septemba 4, 2021 kupitia mitandao ya kijamii ilisambaa video iliyokuwa ikumuonyesha daktari huyo akifumua kidonda cha mgonjwa baada ya kukosa fedha za malipo.