Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma limepata taarifa ya uthibitisho wa daktari kuhusu hali ya akili ya Tito Onesmo Machibya, anayejiita ‘nabii Tito’ kuwa ana ukichaa.
Mtu huyo amekamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kufanya udhalilishaji dhidi ya dini nyingine na kutoa mahubiri yaliyo kinyume na maadili ya nchi.
Akitoa taarifa mbele ya vyombo vya habari jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Mroto amesema kuwa wamepokea taarifa kuwa mtu huyo amewahi kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mwaka 2014 kutokana na kuwa na ugonjwa wa akili. Alisema baada ya kuruhusiwa, ripoti ya daktari inaonesha kuwa alitakiwa kurejea hospitalini hapo lakini hakufanya hivyo.
Aidha, Kamanda Mroto ameeleza kuwa baada ya kumkamata Januari 16 mwaka huu, walimpeleka katika hospitali ya Milembe mjini hapo ambapo daktari alithibitisha kuwa ana ugonjwa wa akili.
“Katika uchunguzi wa awali, Tito Onesmo Machibya anaonekana kama ana historia ya ukichaa kwa mujibu wa taarifa za madaktari. Inaonekana tarehe June 23, 2014 aliwahi kufikishwa Muhimbili akamuona Daktari William,” alisema Kamanda Mroto.
“Tarehe 9 Julai, 2014 alitakiwa kurudi hospitalini hapo lakini mtu huyo hakuweza kurejea,” aliongeza.
Hata hivyo, Kamanda Mroto alieleza kuwa wanamshikilia mtu huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi kufahamu watu anaofanya nao kazi. Pia, kutokana na usalama wake kwani mahubiri anayoyafanya mitaani yanayodhalilisha dini nyingine yanaweza kumsababishia hatari.
Mtu huyo amekuwa akitumia Biblia kutoa mahubiri ambayo yameelezwa kuwa ni yenye tafsiri ya upotoshaji, akisambaza vipeperushi pamoja na vipande vya video kwenye mitandao.