Mwenyekiti wa chama cha wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania, Dkt. Isaack Lema, ametoa ushauri kwa wanaume kujenga utamaduni wa kulia ili kupunguza msongo wa mawazo ambao unaweza kuwasababishia kujiua.
Dkt. Lema ambaye pia ni mwanasaikolojia tiba, ametoa wito huo jana wakati wa mafunzo ya madaktari na wauguzi juu ya afya ya akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
“Wanaume ni wagumu kulia kwa kuhofia kuchekwa na wenzao bila kujua kulia kunapunguza msongo wa mawazo hivyo huishia kujiua kama njia ya kutafuta suluhu ya matatizo.” amesema Lema na kusisitiza ” Mwanaume unapojisikia kulia lia usijibane”
Amesema Wanaume wanaongoza kwa kujiua kuliko wanawake, ambapo moja ya sababu ya kujiua ni kutokulia pia kwani hata wakinusurika katika jaribio la kujiua wakirudia wanafanikiwa.
Amebainisha takwimu zinaonesha kila sekunde watu 40 hujiua duniani na wanaume wanaongoza kujinyonga mara tatu kuliko wanawake.
Aidha, Shirikisho la afya ya akili duniani limetoa takwimu zinazoonesha kuwa kila watu wanne, mmoja anakabiliwa na tatizo la akili lakini pia maeneo ya kazi mtu mmoja kati ya watano anakabiliwa na tatizo la afya ya akili.