Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Tanzania (LATRA) imeyataka mabasi ya usafirishaji abiria maarufu kama ‘daladala’ katika mikoa yote Nchini kubeba watu kulingana na idadi ya siti zilizopo kwenye magari hayo.
Agizo la mamlaka hiyo linakuja mara baada ya Waziri Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kutaka mamlaka hiyo kukaa na wadau wa usafirishaji ili kuja na mapendekezo yatakayo saidia kupunguza usambaaji wa ugonjwa wa Corona nchini.
Aidha kwa mabasi yaendayo haraka (BRT) yametakiwa kubeba idadi ya abiria kulingana na idadi iliyoainishwa kwenye leseni zao na magari ya mizigo hayaruhusiwi kubeba abiria.
Licha ya agizo la kuzia kubeba abiria zaidi ya idadi ya siti ndani ya gari husika, magari hayo yanapaswa kunyunyiziwa dawa kila mwisho wa safari na kuwa na dawa ya kuua wadudu mikononi (hand sanitizer) ili kila abiria apake kabla ya kuingia.
Aidha, Waendesha taksi, pikipiki za magurudumu mawili na matatu wametakiwa kuhakikisha abiria wanapaka dawa ya kuua virusi mikononi (hand sanitizer) kabla ya kupanda kwenye chombo husika.