Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Hassan Dalali, amemtaka kocha mkuu wa Azam FC, Etienne Ndayiragije kuhakikisha anawapa nafasi wachezaji Shaaban Chilunda na Idd Seleman ‘Naddo’ katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Triangle FC  kwenye kikosi cha kwanza ili kuweza kupata ushindi.

Dalali ameeleza kuwa Naddo na Chilunda ni wachezaji muhimu ndani ya kikosi cha Azam FC, ambao kama wakianza, wanaweza kufanya chochote ndani ya dakika 90 ambazo anaamini zitakuwa ngumu sababu ya kila timu inataka kusonga mbele.

Dalali amewamwagia sifa wachezaji hao akieleza kuwa uwepo wao katika timu ya taifa hawana sababu ya kuachwa au kuanzia benchi, kutokana na shauku yao ya kutaka kufunga magoli uwanjani  lengo likiwa ni kuipigania timu yao.

“Kiuhalisia mechi itakuwa ngumu kutokana na Triangle nao watakuwa wanahitaji kupata matokeo, ni vema Ndayiragije akawaanzisha Naddo na Chilunda ambao mimi nawaamini wanaweza kuipa matokeo Azam.

“Nawafahamu vizuri wakiwa uwanjani wanakuwa na njaa ya kucheka na nyavu na uzuri zaidi wapo timu ya taifa, sasa kuna haja gani ya kutokuanza?, Kama Azam wanataka kupindua matokeo wawatumie vizuri wale vijana pale mbele na bila shaka watafanya kile ambacho mimi nakitegemea,” alisema Dalali

Kwa upande mwingine, Dalali amewataka Azam kucheza kwa tahadhari kubwa na kuboresha mapungufu yote yaliyojitokeza katika mechi ya mkondo wa kwanza ili waweze kufanya vema.

Azam itakuwa na kibarua kizito cha mkondo wa pili wa mashindano hayo kitakachopigwa Jumapili ya Septemba 29 kwenye uwanja wa Gibbo uliopo mjini Triangle, Zimbambwe.

Ikumbukwe baada ya Azam kupoteza kwa bao 1-0 katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam, ili iweze kusonga mbele, inapaswa kuibuka na ushindi wa kuanzia mabao 2-0.

Banda aongeza miaka miwili Highlands Park
Serikali yawataka Watanzania kutoa Takwimu sahihi