Ni Rasmi Uongozi wa Azam FC umeachana na Kocha wao wa makipa, Dani Cadena baada ya kumaliza mkataba wake na kutofikia muafaka wa kuongeza mwingine mpya.
Cadena alijiunga na Azam FC, Juni mwaka jana ambapo uongozi wa timu hiyo, ulitangaza ni kocha mzoefu wa kuboresha viwango vya makipa aliwahi kufundisha klabu za Ligi Kuu Hispania (La Liga) Sevilla na Real Betis.
Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa kocha mpya wa Azam anataka kuja na benchi lake la ufundi na hivyo wameanza kuachana na Cadena na watafuata wengine.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Habari, Thabit Zacharia ‘Zaka amethibitisha taarifa hizo kwa kusema Kocha huyo ameondoka baada ya kushindikana makubaliano ya mkataba mpya.
“Kilifanyika kikao kati ya kocha Cadena na uongozi ili kuongeza mkataba mpya, ila ikashindikana hivyo hatakuwa sehemu ya kikosi chetu tena kwa msimu ujao.
“Uongozi unamshukuru kocha Cadena kwa mchango wake tangu alipojiunga nasi mwaka jana, lakini baada ya hapo lazima maisha mengine yaendelee kuhakikisha Azam FC inakuwa na benchi imara kwa ajili ya msimu ujao, hata hivyo kuhusu wengine sina taarifa.”
Kocha huyo ameshafanya kazi China na Saudi Arabia, akiwa na uzoefu mkubwa kwenye soka duniani.