Mshambuliaji kutoka nchini Australia Daniel Arzani hatoweza kushiriki fainali za soka za mataifa ya bara la Asia, zitakazoanza mapema mwaka 2019, kufuatia majeraha ya goti yanayomkabili.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19, alitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Socceroos, ambacho kitakwenda Falme Za Kiarabu (UAE) kutetea ubingwa wa bara la Asia, lakini taarifa zilizotolewa mapema hii leo, zimewahuzunisha mashabiki wengi wa soka nchini Australia.
Arzani alipatwa na majeraha ya goti mwishoni mwa juma lililopita akiwa katika mchezo wa ligi kuu ya soka nchini Scotland, ambapo klabu yake ya Celtic ilikua na kibarua kigumu cha kuikabili Dundee United.
Ilimchukua dakika 20 katika mchezo huo, na baadae madaktari waliamuru asiendelee na mchezo kutokana na hofu iliyokua imetanda, kufuatia jeraha la goti alilolipta.
Hata hivyo haikudhaniwa kama ingemchukua muda mrefu kurejea tena uwanjani, lakini baada ya kufanyiwa vipimo imethibitika Arzani itamchukua miezi miwili hadi mitatu kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mshambuliaji huyo ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo wakati wa faianli za kombe la dunia 2018 zilizounguruma nchini Urusi, alianza kuwafahamisha mashabiki wake kupitia mtandao wa Instagram kwa kuandika; “Sina tena nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya Asia, nimesikitishwa sana na hatua hii, majibu ya vipimo yamedhihirisha ukubwa wa jeraha langu la goti, itanichukua muda mrefu kurejea tena uwanjani”.