Aliyekuwa Kocha wa Walinda Lango Azam FC Daniel Cadena, ameibukia kwa Wekundu wa Masimbazi Simba SC, akitambulishwa kuwa Kocha wa makipa wa kikosi cha wababe hao.
Cadena aliachana na Azam FC siku chache baada ya msimu wa 2022/23 kufikia tamati mwezi uliopita, huku taarifa zikisema Uongozi wa Azam FC ulishindwa kufikia makubaliano ya maslahi yake binafsi, kufuatia mkataba wake wa awali kufikia kikomo.
Leo Alhamis (Julai 06) majira ya mchana Simba SC imemtambulisha Kocha huyo, akiwa ni afisa wa kwanza kutambulishwa katika Benchi la Ufundi la Klabu hiyo kuelekea msimu mpya 2023/24.
Simba SC imemtambulisha Kocha huyo kutoka nchini Hispania kwa kutumia vyanzo vyake vya habari, huku ujumbe uliotumika kumtambulisha ukiandikwa: Karibu Simba SC Kocha mpya wa Magolikipa, Daniel Cadena Ledesma.
Klabu hiyo imepanga kumtambulisha Afisa mwingine wa Benchi la ufundi baadae leo saa kumi jioni, ambaye ataungana na Cadena chini ya utawala wa Kocha Roberto Olivieira ‘Robertinho’.
Utambulisho wa Maafisa wa Benchi la ufundi la Simba SC unachukua nafasi katika kipindi hiki ili kuziba nafasi za walioondoka mwishoni mwa msimu uliopita 2022/23. Walioondoka ni Chlouha Zakaria (Kocha wa Magolikipa), Kelvin Mandla (Kocha Viungo) na Fareed Cassim (Mtaalamu wa Viungo).
Wakati huo huo Klabu ya Azam FC imemtambulisha Kocha wa viungo kutoka nchini Ufaransa Jean-Laurent Geronimi.
Taarifa kutoka klabuni hapo zinaelea kuwa Kocha huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na rasmi anaanza kazi mara moja chini ya utawala wa Kocha Mkuu Youssouph Dabo.