Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy amepuuzia tarehe ya mwisho ya makubaliano ya uhamisho wa Harry Kane iliyopangwa na Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich.
Miamba hiyo ya mjini Munich-Ujerumani ilimuomba Levy kufanya maamuzi haraka ili kufikia mwafaka wa suala la Kane hata hivyo bosi huyo amekwea pipa hadi Marekani kwa ajili ya mapumziko na familia yake kwa muda wa majuma mawili.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti, imefahamika kuwa safari ya bosi huyo haijathibitishwa na inadaiwa lengo ni kukwamisha uhamisho wa Kane.
Aidha Bayern inataka kuwekwa wazi na Spurs kuhusu hatma ya Kane na endapo itashindakana itaachana na Mshambulaiji huyo mwenye umri wa miaka 30.
Bayern ilikuwa na matumaini ya kumtumia Kane kwenye kikosi kitakachocheza fainali ya Kombe la Super Cup dhidi ya RB Leipzig mwishoni mwa juma hili.
Endapo makubaliano hayatakubaliwa Kane anatarajia kubaki Spurs na ataondoka bure mwakani, mkataba wake utakapomalizika kwa mujibu wa ripoti.
Mkurugenzi wa ufundi wa Bayern, Marco Neppe amekuwa mtu muhimu katika mazungumzo ya uhamisho wa Kane baada ya kuonana na familia yake kwa mujibu wa ripoti.
Bosi huyo aliungana na mtendaji wake mkuu Jan-Christian Dreesen kwenye mazungumzo na uongozi wa Spurs jijini London lakini wakagonga mwamba.
Wakati hayo yakiendelea Tottenham imepanga kufanya Usajili wa Mshambuliaji mwingine endapo Kane ataondoka dirisha hili la usajili la kiangazi.
Imeripotiwa kuwa Kane atakuwa tayari kusaini mkataba mpya endapo uhamisho huo utagonga mwamba na atajiandaa na mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu England dhidi ya Brentford mwishoni mwa juma hili.