Klabu ya Arsenal ipo tayari kumuuza mshambuliaji kutoka nchini England Danny Welbeck, baada ya kuona huenda akawa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza msimu wa 2018/19.
Meneja wa klabu hiyo Unai Emery anaamini uwepo wa washambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang, Alexandre Lacazette, Alex Iwobi, Joel Campbell na Lucas Pérez kutamnyima nafasi Welbeck ambaye alisajiliwa klabuni hapo mwaka 2014 akitokea Man Utd.
Tayari klabu za Everton, Bournemouth na Southampton zimeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo, na wakati wowote kuanzia leo zitaanza kuvugana vikumbo kuiwania saini yake kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi siku ya Alkhamis juma hili.
Welbeck tayari ameshajiunga na kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi, baada ya kumaliza likizo ya mapumziko, na amekutana na meneja Unai kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya uwezekano wa kuondoka klabuni hapo.
Tangu alipowasili klabuni hapo mwaka 2015, Welbeck amepata nafasi ya kucheza michezo 80 na kufunga mabao 15.