Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema jeshi la polisi mkoani humo, linawashikilia watuhumiwa wawili, mume na mke kwa kosa la kuikejeli serikali juu ya hatua zake kwenye kukabili mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Cororna.
Akiongea na waandishi wa habari leo Machi 27, 2020, Mambosasa amesema watuhumiwa hao ni Boniface Mwita (29) mkazi wa Tabata na Rosemary Mwita (41) mke wa Boniface ambao walifanya kosa hilo Machi 20, 2020.
“Watuhumiwa hao wakiwa kwenye daladala lenye namba za usajili T119 DKS wakitokea tababta kwenda hospitali ya taifa Muhimbili, walisambaza taarifa za uongo za kupotosha jamii kuhusiana na ugonjwa wa covid 19” Amesema Kamamnda Mambosasa
Na kuongeza “watuhumiwa hao walianza kukejeli lakini wa kitania kwa kusema kwamba serikali inapotosha wananchi kuhusu virusi vya Corona na pia serikali haina fedha kwaajili ya kulisha wanafunzi na ndiyo maana mashule na vyuo vimefungwa kwa kisingizio cha uwepo wa corona”
Amesema jambo hilo liliwakera abiria wenzao ambao waliamuru dereva apeleke gari kituo cha polisi na alipeleka kituo cha central ambapo wanaendelea kushikiliwa na upelelezi umekamilika hivyo watafikishwa Mahakamani.
Kamamnda Mambosasa ametoa rai na onyo kwa watanzania wengine ambao wanafanya kejeli kwa ugonjwa ambao unaangamiza watu wengi duniani, wasichukulie mzaha na kuendelea kupokea taarifa sahihi kutoka kwa Serikali na kuzingatia maelekezo.