Dar24 Media imefanikiwa kutoa jumla ya wateule saba kati ya 91 waliotajwa na Baraza la Habari Tanzania – MCT, kuwania tuzo za EJAT kwa msimu wa 2022/23 rekodi ambayo ni nadra kuwekwa na vyombo vya Habari kwa msimu mmoja.
Rekodi hiyo adimu, inaifanya Dar24 media kuwa chombo cha habari mtandaoni kilichotoa wateule wengi zaidi ambao ni Festo Lumwe, Stanslaus Lambat, Dauka Somba, Zuhura Makuka, Abel Kilumbu, Issa Ramadhani na Heldina Mwingira, kwenye tuzo za mwaka huu, zinazotarajiwa kutolewa Julai 22 jijini Dar es Salaam.
Kazi za Waandishi wote sita walioiwakilisha Dar24 Media, zimepita moja kwa moja katika mchujo na kuingia kwenye fainali hizo ambapo wameungana na Waandishi kutoka vyombo vingine vya Habari kukamilisha orodha ya wateule 91, waliofanikiwa kuingia kwenye tuzo hizo.
Meneja wa Dar24 Media, Abel Kilumbu amesema mafanikio haya makubwa ni matokeo ya ubora na weledi unaozingatiwa na kituo hicho kwenye kuhabarisha na kuelimisha umma ambapo ameongeza kuwa, “hii ndiyo inayotofautisha Dar24 Media na vyombo vingine vya habari.”
Jopo la majaji wanane liliongozwa na Mhariri na Mwandishi wa Habari mbobevu, Mkumbwa Ally ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, walipitia jumla kazi 893 zilizowasilishwa na kuchagua kazi bora zaidi kuingia fainali.