Watu watano wamefariki Dunia na wengine sita kujeruhiwa, kufuatia ajali ya barabarani baada ya lori kubwa la mizigo, kuigonga gari ndogo ya abiria aina ya Noah, wakati likisubiri kuvuka katika daraja la mchepuko la kiyegeya, ambalo lilisombwa na maji mwanzoni mwa mwezi Machi.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Machi 24, 2020, huku chanzo kikielezwa kuwa ni kufeli kwa breki ya Lori na kupelekea vifo vya watu wanne papo hapo na mmoja kufariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, amesema wamepokea majeruhi sita ambao kati yao kuna watoto wawili ambao bado wazazi wao hawahafahamika.
Akizungumza katika eneo la tukio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa, ameeleza kuwa gari hiyo ndogo ilikuwa imebeba abiria kutoka Dumila kuelekea Gairo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta dereva wa Lori kwani alikimbia.