Leo Septemba 11 wanafunzi wa darasa la saba  947,221 wanafanya mtihani wa kumaliza elimu ya shule ya msingi 2019 wenye lengo la kupima uwezo na uelewa wa wanafunzi katika yale yote waliyojifunza kwa kipindi chote cha miaka 7.

Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la mtihani Tanzania, Charles Msonde amesema kuwa katika mtihani huo watahiniwa watafanya masomo matano ambayo ni Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, Sayansi na Maarifa ya jamii.

Ambapo kati ya watahiniwa 947,221 waliosajiliwa kufanya mtihani huo watahiniwa 902,262 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 44,959 kwa lugha ya Kiingereza.

Ameongezea kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalum kwa mwaka huu ni 2,678 kati yao 81 hawaoni, 780 wana uoni hafifu, 325 walemavu, 864 ulemavu wa akili.

Hivyo Baraza limetoa wito kwa wasimamizi wa mtihani huo kuhakikisha wanalinda haki ya watahiniwa wenye mahitaji maalum ametaja haki hizo kuwa pamoja na kuwapa mitihani yenye maandishi makubwa watahiniwa wote wenye uono hafifu lakini pia amesema wenye mahitaji maalum waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine kama ambavyo muongozo wa NECTA unavyoelekeza.

Aidha, Msonde amesisitiza kuwa Baraza halitazifumbia macho shule ambazo zitafanya udanganyifu halitasita kuzichukulia hatua kama ilivyozifutia matokeo baadhi ya shule katika mitihani ya mwaka jana.

Na ameongezea kuwa kwa shule zilizofanya udanganyifu mwaka jana na kufutiwa vituo vyao kuwa vya mtihani wataendelea kufanya mitihani kwenye vituo walivyopangiwa.

 

 

 

 

Neymar kupigwa bei Januari 2020
Makala: JPM ameshinda mtihani na kuliishi ‘neno’, Nape na wenzake ni darasa