Rapa aliyeweka alama kubwa kwenye muziki wa Bongo Fleva hasa mwaka 2016/17, Darassa amejibu tuhuma zinazomfuata mitandaoni kuwa anatumia dawa za kulevya.
Kwa muda sasa, ‘wana mitandao ya kijamii’ wamekuwa wakihusisha ukimya wa rapa huyo na matumizi ya dawa za kulevya huku wengi wakidai ndicho kinachompunguzia kishindo kwenye muziki.
Darassa ambaye hajaweka kitu chochote kwenye mtandao wake wa Instagram tangu Agosti mwaka jana amekanusha tuhuma hizo na kueleza kuwa watu wanachotaka akifanye mitandaoni kuonesha maisha ya starehe sio ambacho atakifanya.
“Nimefanya vitu vikubwa sana, kila mtu atataka kuona nafanya makeke katika mitandao ya kijamii, niko na mwanamke huyu, nipo klabu lakini siyo kitu ambacho nakifanya,” Darassa ameiambia Clouds Fm.
Ameongeza kuwa kwakuwa hafanyi hayo na haonekani katika kumbi za starehe ndio sababu anazushiwa hayo, lakini yeye hafanyi hivyo.
‘Muziki Gani’ ni wimbo wa Darassa ambao madhara yake bado yanaonekana hasa kwa nchi za jirani ambako katika klabu za usiku wimbo huo ni sehemu ya nyimbo za kuuvuta umati kwenye eneo la kucheza (dance floor).