Taasisi binafsi ya Kitanzania, DataVision International kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia Mjema wapo katika mazungumzo yanayotokana na jitahada za DataVision Internation katika mwendelezo wa shughuli zao nyingi za kuisaidia jamii katika nyanja mbalimbali.
Katika mkakati huu, DataVision International wamelenga kuwawezesha madereva wa Bodaboda na Bajaji, kutambulika rasmi na wao kujitambua, ili waweze kupata manufaa makubwa zaidi kutokana na kazi wanayojihusisha nayo .
Kufuatia mpango huo, Mhe. DC Mjema amesema kuwa madereva wa bodaboda ambao ni wa rika mbalimbali wamekuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuibiwa Pikipiki zao, kukosa elimu ya matumizi ya fedha, lakini pia changamoto ya kushindwa kukopesheka kutokana na kazi yao kutokuwa rasmi na hivyo kutambulika na taasisi husika.
Kufuatia hatua ya DataVision International kutumia taaluma yao kutatua changamoto zilizopo katika jamii inayowazunguka, Mhe. Mjema ameupongeza mkakati ambao unakuja na nia ya dhati ya kuwakomboa madereva hao na kuwajengea daraja la maendeleo.
Awali, akizungumza na Mkuu huyo wa Wilaya, Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa DataVision, Bi. Teddy Qirtu amesema kuwa, taasisi hiyo ambayo imejikita katika masuala ya Tehama, Utafiti na Takwimu, Huduma za Malipo na Kadi, pamoja na Mafunzo ya Kitaalam, imefanya utafiti na kugundua kuwa kuna changamoto kadhaa zinazowakabiri wanaoendesha Boda boda na Bajaji ambazo zinachangia kurudisha nyuma maendeleo yao.
Hivyo, Bi. Qirtu amesema kuwa kutokana na uzoefu wa miaka ishirini (20) sasa katika utendaji wana suluhisho sahihi na endelevu la kuwakomboa vijana hao na kuwaneemesha katika kazi yao.
“Moja ya sehemu tutakazojikita ni kuwarasimisha na kuwafanya madereva wa bodaboda watambulike rasmi na hivyo kuweza kunufaika na mipango kadhaa ya kuendeleza jamii yanayotolewa na Serikali kupitia uongozi wa awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambao inahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kufikia katika uchumi wa kati,” amesema Bi. Teddy Qirtu.
Aidha, Bi. Teddy Qirtu akiendelea kuwasilisha wazo la mkakati wa DataVision kwa Mkuu wa Wilaya, Sophia Mjema alisema kampuni hiyo imepanga kutengeneza teknolojia itakayozuia majanga hatarishi wanayokutana nayo pindi wanapotekeleza majukumu yao.
Akiendelea kuelezea kuhusu mkakati huo, Bi. Teddy Qirtu amesema kuwa moja ya sababu iliyowasukuma kuwasaidia waendesha Boda boda na Bajaji ni baada ya kutambua mchango wa sekta hii katika shughuli za maendeleo kufuatia kutoa jawabu la usafiri kwa wananchi kadhaa, hasa wale wa kipato cha wastani.
“Ni kwa ushiriki jumuishi wa kila mmoja wetu ndipo malengo mapana na endelevu ya Serikali na jamii yanaweza kufikiwa. Na hili si jukumu la Serikali peke yake bali linahitaji ushiriki wa sekta binafsi,” ameendelea kusema Bi. Teddy Qirtu.
Taasisi ya DataVision International inaendesha miradi mbali mbali inayofanana na huu ikiwemo mradi wa utambuzi wa wasanii wa Sanaa za ufundi nchini (TACIP) ambao unatekelezwa kupitia Wizara ya Habari Sanaa na Michezo ambapo mlezi wa mradi huo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Kayanza Peter Pinda.