Kampuni ya Kitanzania ya DataVision International inayojishughulisha na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), utafiti na mifumo ya malipo ya kielektroniki, imeshiriki utoaji tuzo za kimataifa za ‘Global Learning X-Prize’ zilizofanyika hivi karibuni jijini Los Angeles nchini Marekani, ambapo washindi waliotengeneza mfumo (app) bora zaidi wa kumsaidia mtoto kujua kusoma, kuandika na kuhesabu bila msaada wa mwalimu walizawadiwa $10 milioni.
Ushiriki wa DataVision International katika utoaji tuzo, katika hafla ya utoaji iliyofanyika Mei 15, 2019, ulitokana na ushiriki wake, kwa kushirikiana na Kampuni ya RTI ya nchini Marekani, kufanya utafiti kwa kutumia program tano zilizochaguliwa kutoka miongoni mwa kampuni zaidi ya 400 kutoka nchi mbalimbali duniani zilizoshiriki katika shindano hilo.
Mradi wa utafiti ulishirikisha watoto 3,000 wenye umri kati ya miaka 7 hadi 10 kutoka wilaya sita za Mkoa wa Tanga. Kupitia utafiti huo uliofanyika mwaka 2017, watoto hao walipewa ‘tablets’ zenye programu (software) maalum inayowasaidia kujifunza wenyewe bila kusaidiwa na mtu yeyote.
Taasisi ya X-Prize, yenye makao yake makuu nchini Marekani, iliyoandaa na kuratibu mashindano hayo, iliyatangaza makampuni mawili kuwa yameshinda yote kwa kulingana alama. Makampuni hayo ni Kitkit School kutoka Korea Kusini na Onebillion kutoka nchini Uingereza. Hivyo, makampuni husika yaligawana $10 milioni kwa lengo la kuwasaidia kuendeleza utengenezaji wa programu zao kwa ufanisi zaidi.
Taasisi ya X-Prize imesema kupitia tovuti yao kuwa asilimia 90 ya watoto walioshiriki katika utafiti huo hapa nchini walikuwa hawawezi kusoma hata neno moja la Kiswahili. Lakini, baada ya kutumia kwa miezi 15 moja kati ya program zilizoshinda, nusu ya watoto hao walikuwa wanaweza kusoma baadhi ya maneno ya Kiswahili.
Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa Kampuni ya DataVision International, William Kihula ambaye alishiriki na kupewa nafasi ya kuzungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo akiambatana na Bi. Bwigane Mulinda, ambaye ni Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni hiyo, alisema, “ushiriki wetu kwenye zoezi hili linaloleta mapinduzi ya utoaji elimu ya awali duniani kwa kutumia teknolojia kukabiliana na uhaba wa walimu unatokana na ufanisi wa kazi zetu kwa kipindi cha miaka 20. Hii, ni heshima kwa Taifa letu na Serikali yetu kwa jinsi ilivyoweka mazingira mazuri ya kuhuisha maendeleo ya teknolojia katika kutatua matatizo ya kijamii.”
“Dunia imeiangalia Tanzania kama kitovu cha mapinduzi ya teknolojia hii muhimu katika kumsaidia mtoto kujua kusoma, kuandika na kuhesabu bila kuingia darasani,” Kihula aliongeza.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni Kusaidia Watoto Duniani (UNESCO), zaidi ya watoto milioni 250 duniani kote hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu huku kukiwa na upungufu mkubwa wa walimu wa elimu ya msingi na sekondari. Utafiti wa Shirika hilo unaonesha kuwa walimu milioni 68.8 wanapaswa kuajiriwa ili kila mtoto mwenye umri husika apate elimu ya msingi na sekondari kufikia mwaka 2030.
“Hili ni tatizo ambalo ni lazima tulitatue. Tunaweza kutumia nguvu ya teknlojia ili watoto kila mahali duniani bila kujali hali zao wanapata fursa ya kujenga maisha yao na kwa ajili yetu sote,” alisema Dkt. Emily Church, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya X-Prize.