Kipa bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2013/2014, David Abdallah Burhan amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Bugando, Mwanza.
Kipa huyo wa Kagera Sugar ya Bukoba alifikishwa hospitalini hapo jana kutoka Bukoba na kwa bahati mbaya asubuhi ya leo ameaga dunia.
Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime amesema Burhan alikuwa anasumbuliwa na Malaria.
Mexime alisema matatizo hayo yalianza wakati wamekwenda Singida kucheza na wenyeji, Singida United mechi ya Kombe la Shirikisho.
Alisema alipanga kumuanzisha David Burhan katika mchezo huo, lakini hali yake ikabadilika ghafla hivyo akampanga kipa mwingine, Juma Kaseja badala yake.
“Tumecheza mechi, baada ya mechi wakati tunarudi, tunafika Biharamulo, macho yake yakaanza kubadilika yakawa ya njano, ikabidi alazwe pale, kesho yake akahamishiwa hospitali ya mkoa wa Kagera, ambako baada ya kupimwa wakasema apelekwe Bugando,”alisema Mexime.
Amesema uongozi wa Kagera Sugar ukafanya utaratibu wa haraka wa kumchukulia ndege kwenda Mwanza ambako alifika jana na kuanza matibabu kabla ya kufariki dunia leo.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kurejeshwa kwao Iringa na kuhusu mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Mexime amesema kwamba hawajajua kama utachezwa au la.
“Sasa hivi ndiyo tunakwenda kwenye kikao cha kabla ya mechi, tukifika huko ndiyo tutajua, ila kwa kweli upande wetu wachezaji wote wameshtushwa mno na taarifa hizi na sidhani kama wapo tayari kwa mechi ya leo,”alisema.
Burham alijiunga na Kagera Sugar msimu huu akitokea Maji Maji ya Songea, ambayo nayo ilimsajili akitokea Mbeya City. Huyo ndiye aliyekuwa kipa wa kwanza Mbeya City wakati inapanda Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita chini ya kocha Juma Mwambusi na akawa kipa bora wa msimu wa 2013/2014.