Beki David Alaba hakuwa sehemu ya mazoezi ya mwisho ya kikosi cha Real Madrid, kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City.
Miamba hiyo itakutana leo mjini Madrid, kumaliza ubishi wa nani anatinga hatua ya Fainali ya michuano hiyo, huku Manchester City ikiongoza kwa mabao 4-3, walioyapata katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza mjini Manchester juma lililopita.
Kukosekana kwa Alaba katika amzoezi ya mwisho ya The Galacticos, kunadhihirisha ataukosa mchezo wa leo Jumatano (Mei 04).
Beki huyo mahiri, aliyesajiliwa kwa uhamisho huru msimu uliopita baada ya kumalizika kwa mkataba wake Bayern Munich, amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya ulinzi ya Kocha Carlo Ancelotti msimu huu na amecheza michezo 45 katika michuano yote.
Hata hivyo, Alaba alitolewa katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City juma lililopitia, ambapo taarifa zilzieleza kuwa, alikuwa na tatizo la misuli ya paja, na haijafahamika iwapo atarejea kwa wakati, huku pia alikosa mchezo dhidi ya Espanyol, Jumamosi (April 30).
Madrid wanawania nafasi ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayofanyika Mei 28 mjini Paris.
Gareth Bale pia hakushiriki mazoezi kamili, huku Eden Hazard akiendelea kupata nafuu kutokana na jeraha lake la kifundo cha mguu.