Mlinda Lango wa Manchester United, David de Gea, amekubali kuongezwa mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake mjini Manchester.
De Gea ataongeza mkataba wa muda mrefu baada ya kufikia mwafaka na uongozi wa Man United.
Hata hivyo, pamoja na kukubali kuongezwa mkataba mpya, Mlinda Lango huyo ameonyesha hofu ya kutokuwa na uhakika wa kuwa chaguo la kwanza msimu ujao 2023/24.
Taarifa kutoka katika mtandao wa klabu ya Manchester United, zimeeleza kuwa, makubaliano ya pande mbili yamekamilika na wakati wowote kuanzia sasa De Gea atatia saini mkataba mpya.
Taarifa hiyo imesema kuwa baada ya kutia saini mkataba mpya, De Gea atalipwa mshahara wa pauni 350,000 kwa juma, iwapo Man United itafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu ujao.
Awali, De Gea mwenye umri wa miaka 32 alikuwa akihusishwa kutaka kuondoka kikosini.
Pamoja na De Gea, United inaendelea kutafuta saini za Walinda Lango wengine wapya akiwemo Diogo Costa wa FC Porto ya Ureno na David Raya anayekipiga Brentford ya England.