Klabu ya Sunderland imemsajili beki wa pembeni kutoka nchini Costa Rica Bryan Oviedo pamoja na kiungo wa Ireland Kaskazini Darron Gibson wakitokea Everton.

Usajili wa wawili hao umeripotiwa kufanyika kabla ya dirisha la usajili kufungwa hii leo, kufuatia msukumo mkubwa uliowekwa na meneja David Moyes.

Uongozi wa klabu ya Sunderland umetoa taarifa za kumsainisha mkataba wa miaka mitatu Oviedo na atakaa Stadium of Light hadi mwaka 2020, huku akichukua nafasi ya Patrick van Aanholt ambaye amesajiliwa na klabu ya Crystal Palace.

Moyes alimsajili beki huyo mwenye umri wa miaka 26 alipokua mkuu wa benchi la ufundi la Everton kabla ya kutimkia Old Trafford mwaka 2013 kuchukua nafasi ya Sir Alex Ferguson.

Gibson mwenye umri wa miaka 29, naye aliwahi kucheza soka chini ya utawala wa Moyes alipokua Goodison Park na amekubali kusaini mkataba wa miezi 18 (Mwaka mmoja na nusu).

Oviedo amecheza michezo saba akiwa na klabu ya Everton kwa msimu huu wa 2016/17.

Usajili wa wachezaji hao wawili unaongeza idadi ya waliosajiliwa Stadium Of Lights huku historia zao zikionyesha waliwahi kupita katika klabu ya Everton.

 

Wachezaji hao ni Joleon Lescott,  Jack Rodwell, Steven Pienaar pamoja na Victor Anichebe.

Mwakyembe aanza kutekeleza kwa vitendo agizo la JPM
Matokeo kidato cha nne yatangazwa,ufaulu wazidi kupaa