Baada ya kuanza na matokeo ya sare ya bao moja kwa moja katika harakati za kuwania ubingwa wa barani Ulaya msimu huu wa 2016/17 dhidi ya mabingwa wa soka wa Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG), meneja wa Arsenal Arsene Wenger amemwagia sifa kedekede mlinda mlango wake kutoka nchini Colombia  David Ospina.

Ospina alionekana kuwa shujaa wa Arsenal katika mchezo huo uliounguruma usiku wa kuamkia hii leo jijini Paris, kwa kufanikiwa kuokoa michomo mikali iliyokua ikielekezwa langoni mwake wakati wote.

Wenger aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo kumalizika kwenye uwanja wa Parc des Princes, hana budi kumshukuru Ospina kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wote na anaamini mlinda mlango huyo amedhihirisha ubora wake.

Wenger alisema Ospina alikua shujaa wa kikosi chake na wakati mwingine hakuamini pale alipoona anafanya kazi ya ziada ya kuokoa mipira iliyokua inawaaminisha mashabiki wengi huenda ingetinga nyavuni.

“Ninapaswa kumshukuru kwa uwezo wake mkubwa aliouonyesha japo naamini uwezo wake siku zote umekua ukionekana hata tukiwa katika mazoezi.” Alisema Wenger

Hata hivyo mzee huyo ametamba kuwa na walinda mlango bora katika kipindi hiki, jambo ambalo amekiri linamfariji na kumuaminisha hakutokua na shaka endapo mmoja wao atakutwa na matatizo ya kiafya.

“Ninao walinda mlango wawili wenye viwango vikubwa,”

“Ninaweza kumteua yoyote kukaa langoni bila kujali mchezo unaotukabili.” Aliongeza babu huyo kutoka nchini Ufaransa.

David Ospina (right) was preferred to Petr Cech for ArsenalWalinda mlango wa Arsenal David Ospina (kulia) na Petr Cech kabla ya mchezo dhidi ya PSG.

Katika mchezo huo PSG walitangulia kupata bao la mapema lililofungwa na mshambuliaji wao kutoka nchini Uruguay Edinson Cavani katika dakika ya kwanza, lakini Alexis Sanchez aliisawazishia Arsenal katika dakika 77.

Arsenal na PSG walicheza mchezo huo wa kwanza katika kundi A, ambalo pia lina klabu za FC Basel na Ludogorets Razgrad.

Matokeo ya mchezo kati ya FC Basel na Ludogorets Razgrad, ni sare ya bao moja kwa moja, hatua ambayo imelifanya kundi hilo kukosa kiongozi kwa kigezo cha kupata point tatu.

John Terry Kuwakosa Liverpool
FA Yamuweka Kikaangoni Mark Hughes