Kiungo wa zamani wa Manchester City, David Silva, anaamini kuwa Arsenal pekee ndiyo wanaweza kuwania taji la Premier League msimu huu mbele ya Man City.
Kocha Mikel Arteta na vijana wake wa Arsenal, msimu uliopita walipambana na Pep Guardiola kuwania ubingwa na wa Premier, wakapishana kwa pointi tano wakati Man City ikiwa bingwa.
Msimu uliopita Arsenal walimaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Premier nyuma ya Man City, huku ya tatu ikishikwa na Manchester United na ya nne Newcastle United.
Arsenal msimu huu imefanikiwa kupata ushindi wa mechi tatu kati ya nne, huku Silva akiamini kwamba usajili wa Declan Rice utampa nguvu Arteta ya kuwania ubingwa wa Premier League.
Silva alisema: “City wana timu nzuri yenye wachezaji bora, huu ni msimu wa nane kwa Pep ndani ya Man City. Kwanza ilikuwa ni kuzoea Premier league, ila hivi sasa amekuwa hakamatiki.
“Arsenal ni timu pekee ambayo naona inaweza kushindana na City kuwania taji, kwa wengine sifikirii.
“Msimu uliopita niliangalia mechi za City zote za Ligi ya Mabingwa Ulaya, nilifurahi kuona wakifanya vizuri, hakika walistahili kutwaa mataji yote matatu.”