Gwiji wa Klabu Bingwa nchini England Manchester City, David Silva ametangaza kustaafu kucheza soka akiwa na umri wa miaka 37, siku chache baada ya kuumia goti.

Silva alikuwa amepanga kuendelea na soka katika klabu ya Real Sociedad, lakini jeraha la goti alilolipata kabla ya msimu mpya limetishia kumweka nje kwa muda mwingi wa msimu ujao na kuamua kubadili mipango yake.

“Leo (jana) ni siku ya huzuni kwangu,” alisema Silva katika ujumbe wa video uliotumwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Leo (jana) ni wakati wa kuaga kile ambacho nimejitolea maisha yangu yote. Nitakumbuka sana. Asante kwa kunifanya nijisikie nyumbani.

“Silva alianza maisha yake ya soka kule Valencia, ambapo alicheza mechi 168 na kubeba kombe la Hispania, lakini ubora wake ulikuja City, ambao alijiunga nao mwaka 2010 na kuwa gwiji wa klabu.

Kiungo huyo mbunifu alikuwa sehemu muhimu ya timu ya City ambayo iliyonyanyua taji la kwanza la ligi kuu ya England msimu wa 2011-12 katika siku ya mwisho ya msimu.

Alishinda mataji mengine matatu ya ligi kuu akiwa na City, mawili ya mwisho akiwa chini ya kocha Pep Guardiola.

Silva amewekewa sanamu nje ya uwanja wa Etihad pamoja na wachezaji wenzake wa zamani Vincent Kompany na Sergio Aguero.

Silva aliondoka City mwaka 2020 baada ya kucheza mechi 436 na kurejea La Liga katika Klabu ya Sociedad.

Young Africans yashtukia Kimataifa
Robertinho afurahia uwezo Simba SC