Mwandishi na muimbaji wa muziki mwenye uraia wa Nigeria na Marekani David Adedeji Adeleke, al maarufu Davido ametoa orodha ya vituo vya yatima kote nchini Nigeria ambavyo amefanikiwa kuvipatia jumla ya naira 250,000,000 ikiwa ni sawa na dola za kimarekani millioni 600,814.25.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kupitia ukurasa wa Twitter wa muimbaji huyo zinasema kuwa kuwa alitimiza ahadi yake ya mwaka 2021, alipopokea mamilioni ya naira katika kipindi cha saa 72 baada ya kuushirikisha umma mawazo yake ya kutaka kuchangisha kwa ajili ya watoto yatima na akatoa nambari ya akaunti yake ya benki kwenye mitandao ya kijamii wakati wa maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa.
“Kama nilivyoahidi, kamati ya wanaume watano ya usamabazaji wa pesa iliwekwa. Tangu ilipozinduliwa, wajumbe wa kamati hii wamefanya kazi bila kuchoka kuhakikisha wanakusanya majina na taarifa zilizopo na kuhakikisha vituo vya yatima. Ninafuraha kutangaza kuwa utoaji wa pesa umekamilika,” ilieleza sehemu ya taarifa yake.
Kulingana na Davido, alifikiria kuushirikisha umma rekodi hiyo ili kuonyesha uwazi wa malengo yake ya awali.
“Hadi sasa jumla ya Naira 250,000,000 zimetolewa katika vituo 292 vya yatima,” ilifichua taarifa yake, na kuongeza kuwa, “Katika moyo wa kuwa na uwazi nilidhani ni busara kuwafahamisha wanaoniunga mkono, mashabiki, marafiki na familia yaliyofikiwa kuhusiana na hili.”
Davido alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa marafiki ambao aliwaelezea kama wenye maadili ya juu na misimamo.
“Ningependa kusema asante sana kwa kila mmoja ambaye alifanikisha hili, kamati ya watu wenye maadili mema na msimamo ambao walijitolea muda wao kuhakikisha jukumu hili linafanyika, familia yangu nzuri, marafikina wengine wanaotakamema,”alisema.