Klabu ya Tottenham Hotspur ya jijini Lonodn-England, imekubali kumpiga bei Davinson Sanchez kwenda Spartak Moscow.
Klabu hizo mbili zimefikia makubaliano ya ada ya Pauni 13 milioni kwa ajili ya huduma ya beki huyo wa kati.
Uhamisho huo sasa umebaki kwa mchezaji kuamua na Spurs inasikilizia atakachoamua.
Makubaliano binafsi baina ya mchezaji na Spartak Moscow bado hayajafikiwa, huku klabu hiyo ilishika nafasi ya tatu kwenye ligi ya Russia msimu uliopita, walipigwa marufuku michuano ya Ulaya baada ya Russia kuivamia kivita Ukraine.
Sanchez amekuwa kwenye kikosi cha Spurs tangu 2017, aliponaswa kutoka Ajax kwa Pauni 42 milioni. Alicheza mechi 205 katika klabu hiyo na kufunga mabao matano.
Hata hivyo, alianzishwa kwenye mechi nane tu za Ligi Kuu England baada ya kuwekwa kando kutokana na ubora wake kushuka.
Kocha mpya Ange Postecoglou ameripotiwa kuwa tayari kumpiga bei staa huyo wa kimataifa wa Colombia.
Kumekuwa na ofa nyingine kutoka klabu za Real Betis, Sevilla na Galatasaray zinazohitaji saini ya mchezaji huyo.
Spurs wao tayari wameshaanza kusaka mrithi wa Sanchez na inaweza kumnasa Clement Lenglet kwa dau la jumla baada ya mkopo wa msimu uliopita.
Staa wa Bayer Leverkusen, Edmond Tapsoba, wa Wolsburg, Micky van de Ven na mkali wa Fulham, Tosin Adarabioyo ni wachezaji wengine waliopo kwenye rada za miamba hiyo ya London.