Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) limezindua mfumo mpya wa mawasiliano ambao unalenga kumrahisishia mteja kupata na kutoa taarifa zinazohusu huduma hiyo kwa haraka zaidi.
Huduma hiyo mpya sasa itapatikana kwa wakazi wote wa jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA) wa DAWASCO, Bw. Kiula Kingu amesema lengo kuu la mfumo huu ni kumweka mteja karibu kihuduma na kila mwananchi ana uwezo wa kutumia mfumo huo katika simu yake kupitia mitandao yote ya simu za mikononi nchini.
Kingu ameongeza kuwa ili mteja kunufaika na mfumo huu anatakiwa kuhakikisha ana simu ya mkononi ya “Smartphone” ambayo itamwezesha kupakua mfumo huo mpya wa DAWASCO, kisha kujisajili kwa kuingiza akaunti namba yake ya DAWASCO ambapo baada ya kufuata hatua zote za kujisajili mteja atatumiwa neno la siri ambalo litamwezesha kuingia na kupata taarifa husika.
“Sisi Dawasco tumeona haja ya kujiboresha na kwenda sawa na teknolojia kwa kumletea mteja wetu mfumo rahisi ambao utamwezesha kupata taarifa zetu kupitia simu yake ya mkononi muda wowote,”amesema Bw. Kingu.